Print Sermon

Kusudi la tovuti hii ni kuandaa makala ya mahubiri na mahubiri ya video bila malipo kwa Wachungaji na Wanamisheni duniani kote, hasa katika Ulimwengu wa Tatu, sehemu ambazo kuna uchache ama ukosefu wa vyuo vya theolojia au shule za Bibilia.

Makala ya mahubiri haya na video ufikia kompyuta 1,500,000 katika zaidi ya nchi 221 kila mwaka kupitia tovuti www.sermonsfortheworld.com. Mamia ya watu wengine hutazama video kupitia You Tube, lakini wao huondoka kutoka YouTube na kuingia katika tovuti yetu. YouTube huwaelekeza watu katika tovuti yetu. Makala ya mahubiri haya yanatolewa kwa lugha 46 kwa kompyuta takriban 120,000 kila mwezi. Makala ya mahubiri haya hayana hatimiliki, hivyo wahubiri wanaweza kuyatumia bila idhini yetu. Tafadhali bonyeza hapa ili ujue jinsi unavyoweza kutuma mchango wako kila mwezi ili utusaidie katika kazi hii kuu ya kueneza Injili kote ulimwenguni.

Kila unapomwandikia Dkt. Hymers kila wakati mjulishe nchi unayoishi, la sivyo hawezi kukujibu. Barua pepe ya Dkt. Hymers ni rlhymersjr@sbcglobal.net.




JASHO YA DAMU

THE BLOODY SWEAT
(Swahili)

na Dkt. R. L. Hymers, Jr.

Mahubiri yaliyohubiriwa katika Baptist Tabernacle kule Los Angeles
Siku ya Bwana, Februari 18, 2018
A sermon preached at the Baptist Tabernacle of Los Angeles
Lord’s Day Evening, February 28, 2018

“Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22:44).


Mizingi ya ujumbe huu ni mahubiri mawili makuu ya C. H. Spurgeon, “Maumivu katika Bustani” (Octoba 18, 1874) na “Gethsemane” (Februari 8, 1863). Nitakupa kwa muhtasari mahubiri haya mawili ya kazi bora ya mkuu wa wahubiri. Hakuna chochote kilicho cha awali hapa. Nimeyarahisisha mahubiri haya kumfaa mtu wa kisasa asiye na masomo mengi. Mawazo haya nimeyakusanya kutoka kwa mahubiri ya mhubiri huyu mkuu, na ninakuletea mahubiri haya nikitumaini kwamba maelezo ya Spurgeon kuhusu Kristo katika Bustani ya Gethsemane yataishika nafsi yako na kubadilisha maisha yako ya milele.

Yesu alikula chakula cha Pasaka na akasherehekea Meza ya Bwana na Wanafunzi wake. Halafu akaenda nao katika Bustani ya Gethsemane. Kwanini alichagua kuanzia maumivu Yake Gethsemane? Ilikuwa kwa sababu dhambi ya Adamu ilituangamiza katika bustani, Bustani ya Edeni; hivyo Adamu wa mwisho alinuia kuturejesha kupitia bustani nyingine, Bustani ya Gethsemane?

Kristo mara nyingi alienda Gethsemane kuomba. Ni mahali ambapo alienda mara nyingi. Yesu alikusudia tuone kwamba dhambi zetu zilibadilisha kila kitu kumhusu kuwa huzuni. Mahali ambapo alifurahia zaidi ndipo alipoitwa kuteseka zaidi.

Ama anaweza kuwa alichagua Gethsemane kwa sababu ilimkumbusha nyakati alipoomba pale. Ni mahali ambapo Mungu alimjibu mara nyingi. Pengine Alihisi alihitaji kukumbuka majibu ya Mungu ya maombi kwa wakati huo, alipokuwa akiingia katika maumivu.

Pengine sababu kuu ya kwenda Gethsemane ni kwamba yalikuwa mazoea kwake kwenda pale, na kila mtu alijua.Yohana anatuambia, “Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake” (Yohana 18:2). Yesu makusudi alienda mahali ambapo alijua watamkamata. Wakati ulipofika wake wa kusalitiwa, Alienda “Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni” (Isaya 53:7). Hakujificha kwa maaskari wa kuhani mkuu. Hakuhitaji kutafutwa kama mwizi, ama kusakwa na wapelelesi. Yesu alienda kwa hiari mahali ambapo alijua msaliti angempata kwa urahisi na maadui Wake kumkamata.

Na sasa tunaingia katika Bustani ya Gethsemane. Ni jinsi gani usiku huu ulivyo wa giza na kuogofya. Kwa hakika tunaweza kusema pamoja na Yakobo, “Mahali hapa panatisha kama nini!” (Mwanzo 28:17). Tunapotafakari kuhusu Gethsemane, tutafikiria kuhusu maumivu ya Kristo, na nitajaribu kujibu maswali matatu kuhusu huzuni Yake katika Bustani.

I. Kwanza, Ni nini iliyosababisha unchungu na maumivu ya Kristo katika Gethsemane?

Maandiko yanatuambia ya kwamba Yesu alikuwa “Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko” (Isaya 53:3), lakini hakuwa na unyogovu katika nafsi Yake. Alikuwa na amani kuu ndani yake ya kwamba angesema “amani yangu nawapa” (Yohona 14:27). Sifikiri nimekosea ninaposema Yesu alikuwa mwenye amani, na mtu aliyekuwa na furaha.

Lakini pale Gethsemane yote yalibadilika. Amani Yake imeondoka. Furaha Yake imegeuzwa kuwa huzuni inayovurugavuruga. Anapoteremka mwinuko wa kilima kutoka Yerusalemu, kuvuka kijito cha kidroni, kuelekea Gethsemane, Mwokozi aliomba na aliongea kwa ukunjufu (Yohana 15-17).

“Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake” (Yohana 18:1).

Yesu hakuzungumza neno lolote kuhusu kuhisi huzuni au unyogovu wakati wa maisha Yake yote. Lakini sasa, anapoingia katika Bustani, mambo yote yamebadilika. Alilia, “ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke” (Mathayo 26:39). Kwa maisha Yake yote, Yesu hakutamka neno lolote lililoashiria huzuni au unyogovu, bado hapa anahema, na kutokwa na jasho ya damu, na akasema, “Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa” (Mathayo 26:38). Ni nini kilichokasoro nawewe, Bwana Yesu, Ya kwamba lazima uhangaike sana?

Ni wazi kwamba huzuni hii na taabu haikusababishwa na uchungu katika mwili Wake. Hapo awali Yesu akuwahi kulalamika kuhusu shinda yeyote ya mwili. Alihuzunika wakati rafiki Yake Lazaro alikufa. Bila shaka alihuzunika wakati maadui Wake walisema yeye ni mlevi, na wakati walimlaumu ya kwamba anafurusha mapepo kupitia nguvu za Shetani. Lakini alistahimili haya yote na akayapita. Yalikuwa nyuma Yake. Lazima kuwe kulikuwa na jambo lililokuwa na makali kuliko uchungu, kali kuliko shutuma, la kutisha zaidi kuliko msiba, ambalo kwa wakati huu lilimkamata Mwokosi, na likamfanya “kuhuzunika na kusononeka” (Mathayo 26:37).

Unafikiria ya kwamba ilikuwa woga wa kifo, na hofu ya kusulubiwa? Wafia dini wengi wamekufa kishujaa kwa sababu ya imani yao. Ni jambo la kutomheshimu Kristo kufikiria ya kwamba hakuwa na ushujaa kama wao. Bwana wetu hastahili kufikiriwa ya kwamba alikuwa hafifu kuliko wafia dini wake walio mfuata hadi kufa! Pia, Bibilia inasema, “ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu…” (Waebrania 12:2). Hakuna yeyote angepigana na uchungu wa kifo kuliko Yesu. Hiyo aingekuwa sababu ya maumivu Yake katika Bustani.

Pia, Siamini ya kwamba maumivu ya Gethsemane yalisababishwa na shambulio la Shetani ambalo halikuwa la kawaida. Mwanzo wa huduma Yake, Kristo alipitia mapambano makali ya Ibilisi wakati alikuwa jangwani. Bado hatujaona mahali imeandikwa “alikuwa na maumivu” kule jangwani. Katika yale majaribu ya jangwani hakukuwa na jambo kama jasho ya damu ya Gethsemane. Wakati Bwana wa malaika alisimama uso kwa uso na Shetani, hakutamka maneno mazito ya kilio na machozi, akisujudu na kumwoma Baba. Ukilinganisha na hili, mapambano ya Kristo na Shetani yalikuwa rahisi. Lakini maumivu ya Gethsemane yalimjeruhi nafsi Yake na karibu yamuue.

Ni nini ilisababisha maumivu yake, wakati huo? Huu ulikuwa wakati ambapo Mungu alimuingiza katika huzuni kwa ajili yetu. Ni wakati huu Yesu alistahili akichukue kikombe fulani kutoka kwa mkono wa Baba. Alikuwa ana kiogopa. Hivyo unaweza kuwa na hakika kwamba kilikuwa cha kuogofya zaidi kuliko uchungu wa mwili, kutoka wakati huo hakurudi nyuma. Ilikuwa mbaya kuliko kuwa na watu ambao wamekukasirikia – kutoka wakati huo hakugeuka kando. Ilikuwa ya kuogofya kuliko majaribu ya Shetani – ambayo aliyashinda. Lilikuwa jambo la kushangaza na la kuangaisha, kustaajabisha na kutisha–lililomjia kutoka kwa Mungu Baba.

Hii inaondoa shaka yote kuhusu ni nini ilisababisha maumivu yake:

“Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.” (Isaya 53:6).

Sasa yeye amechukua laana ambayo ilistahili ituangukie. Alisimama na kuteseka kwa ajili ya mwenye dhambi. Hiyo ndiyo siri ya maumivu ambayo siwezi kueleza zaidi ya hivi. Hakuna mawazo ya mwanadamu yanaweza kufahamu mateso haya kikamilifu.

‘Hii ni kwa Mungu, na Mungu pekee,
Kwamba huzuni yake inafahamika vyema.
   (“Mateso Yako yasiyojulikana” na Joseph Hart, 1712-1768).

Kondoo wa Mungu amechukua dhambi za wanadamu katika mwili wake, na uzito wa dhambi zetu uko juu ya nafsi Yake.

“Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa” (I Petro 2:24).

Naamini ya kwamba dhambi zetu zote ziliwekwa juu ya “mwili wake” pale Gethsemane, na ya kwamba alichukua dhambi zetu msalabani siku iliyofuata.

Pale katika Bustani Kristo alifahamu ilikuwa na maana gani kuwa mtu-anayebeba dhambi. Akawa mtu aliyesukumiwa makosa ya mwingine, Akazichukua dhambi za Israeli kichwani mwake, kuchukuliwa na kufanywa kafara ya dhambi, kuchukuliwa nje ya kambi na kuteketezwa kabisa na moto wa gadhabu ya Mungu. Sasa umeona kilichomfanya Kristo ajikunje kutokana na hili? Lilikuwa jambo la kuogofya kwa Kristo kusimama mbela za Mungu mahali pa mwenye dhambi – kama vile Luther angesema, kuangaliwa na Mungu kana kwamba Yeye ndiye wenye dhambi wote wa dunia. Kwa sasa Yeye ameingia katikati ya kisasi na gadhabu yote ya Mungu. Amechukua hukumu ambayo ingemwangukia mwanadamu mwenye dhambi. Kuwa katika nafasi hii lazima liwe jambo ambalo lilimhangaisha Kristo.

Halafu, pia, adhabu ya dhambi ikaanza kumwangukia pale Bustani. Kwanza, dhambi yenyewe ilimwangukia, halafu adhabu ya dhambi. Hayo hayakuwa mateso madogo yaliyotimiza haki ya Mungu kwa ajili ya dhambi za watu. Kamwe siogopi kutia chumvi yale Bwana wetu alivumilia. Jahanamu yote ilimiminwa katika hicho kikombe alichokinywa.

Taabu iliyovunja roho ya Mwokozi, bahari kuu isiyopimika ya uchungu iliyopata nafsi ya mwokozi katika kifo chake cha kidhabihu, ni jambo linaloshinda akili na sistahili kuendelea sana, ama mtu atanilaumu ya kwamba ninajaribu kueleza mambo yasiyoelezeka. Lakini hili nitalisema, ule munyunyizio kutoka kwa dhoruba hii kuu ya dhambi za mwanadamu, uliokuwa unamwangukia Kristo, ulimbatiza katika jasho ya damu. Kuchukuliwa kama mwenye dhambi, kuadhibiwa kama mwenye dhambi, ingawa hakutenda dhambi yeyote – hii ndio iliyosababisha maumivu ambayo tunayazungumzia katika haya maandiko.

“Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22:44).

Sasa tunakuja kwa swali la pili.

II. Pili, maana ya Jasho ya Damu ya Kristo ilikuwa nini?

Ellicott anatuambia ya kwamba uhakika wa jasho ya damu ni “fikira inayopokelewa kwa kawaida” (Charles John Ellicott, Mafafanusi ya Bibilia nzima, sehemu ya VI, k. 351). Anaendelea kuonyesha kwamba “Msemo huu ‘jasho ya damu,’ [ulikuwa] umejulikana kama dalili ya kuishiwa nguvu kupita kadiri katika Aristotle ” (ibid.). Tangu wakati wa Augustine hadi siku ya leo wafafanusi wengi wameshikilia ya kwamba haya maneno “kama yalivyokuwa” yanaonyesha hasa ilikuwa damu halisi. Tunaamini pia Kristo kwa kweli alitokwa na jasho ya damu. Hata ingawa hili si jambo la kawaida, imeshuhudiwa kwa watu wengine nyakati mbalimbali katika historia. Katika vitabu vya kale vya dawa vya Galen, na vingine vya hivi karibuni, kuna habari zilizoandikwa za watu ambao baada ya kuwa na muda mrefu wa udhaifu walitokwa na jasho ya damu.

Lakin hali hii ya Kristo kutokwa na jasho ya damu ni ya kipekee. Hakutokwa tu na jasho ya damu, lakini yalikuwa matone makubwa ama “vidonge,” vikubwa, na matone mazito. Hii haija onekana katika hali zingene zote. Damu wakati mwingine imeonekana katika jasho ya watu wagonjwa, lakini hayajawahi kuwa matone makubwa. Halafu tunaambiwa ya kwamba haya matone makubwa ya damu hayakupenya dani ya nguo zake, lakini “yalikuwa yanaanguka chini.” Hapa Kristo ako peke Yake katika historia ya utabibu. Ako katika afya nzuri, mtu aliye na umri wa karibu miaka thelathini na mitatu. Lakini shinikisho kutoka kwa akili kwa sababu ya uzito wa taabu yake, na kule kupopotoa kwa nguvu zake, kulilazimisha mwili wake kufanya jambo lisilo la kawaida na kufungua matundu ya jasho na matone makubwa ya damu yakatoka na kuanguka chini. Hii inaonyesha jinsi uzito wa dhambi ulivyokuwa mkuu juu yake. Ilimbana Mwokozi hadi ngozi yake ikatokwa na damu.

Hii inaonyesha jinsi mateso ya Kristo yalivyokuwa ya kujitolea, kwa sababu bila kisu damu ilitoka yenyewe. Madaktari wa matibabu husema ya kwamba watu wengi wakipitia hali ya kutisha, damu ukimbia kwa moyo. Machavu yanageuka rangi; kunakuwa na hali kama ya kuzimia; damu imeingia na dani. Lakini angalia Mwokozi wetu katika maumivu yake. Anajisahau kiasi cha kwamba damu yake, badala ya damu yake kwenda dani kumlisha, inapelekwa nje na kuanguka chini. Kule kumwagika kwa Damu yake chini kunatoa taswira ya ukamilifu wa wokovu unaotolewa kwako bure. Kama vile Damu ilitiririka kutoka kwa ngozi yake, hivyo unaweza oshwa kutokana na dhambi zako bure unapomwamini Yesu.

“Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22:44).

Jasho ya damu ilikuwa matokea ya huzuni iliyokuwa katika nafsi yake. Uchungu katika moyo ndio uchungu ulio mbaya kabisa. Huzuni na unyogovu ndio majonzi makuu. Wale ambao wamepitia unyogovu wa kina wanaweza kuwaeleza ukweli huu. Katika Mathayo tunasoma ya kwamba akaanza “kuhuzunika na kusononeka” (Mathayo 26:37). “Kusononeka” – musemo huu una maana nyingi. Unaeleza mawazo ambayo yamejawa na huzuni, kiasi cha kwamba hayawezi kuwa na fikira nyingine. Nafasi yake kama mtu anayebeba dhambi zetu iliondoa mawazo yake yoke kutoka kwa mambo mengine yote. Alirushwa rushwa mbele na nyuma katika bahari ya mawazo yaliyosumbuka. “Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.” (Isaya 53:4). “Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika” (Isaya 53:11). Moyo wake ulimlemea. Alijawa na hofu kuu na fadhaa. Alikuwa “amesononeka.” Msomi Puritan Thomas Goodwin alisema, “Maneno haya yana ishara ya mwanguko, ukosefu, na kule kudidimia kwa roho, kama vile yanavyowapata watu wakiwa wagonjwa na wanapozimia.” Ugonjwa wa Epafrodita, ambao ulikuwa karibu kusababisha kifo chake, ulijulikana kwa jina hilo hilo. Hivyo, tunaona nafsi ya Kristo ilikuwa gonjwa na yenye kuzimia. Jasho yake ilisababishwa na kuishiwa nguvu. Baridi, na jasho yenye kunata ya watu wanaokufa inatokana na udhaifu wa miili yao. Lakini jasho ya damu ya Yesu ilitokana na kule kufa kwa dani kwa nafsi yake, ikiwa imelemewa na dhambi zetu. Alikuwa katika hali ya kutisha ya kuzimia-kinafsi, na akapitia hali ya kifo ndani yake, ikiambatana na kutokwa na damu mwili wote. “Alisononeka”sana.

Injili ya Marko inatuambia ya kwamba alikuwa na “huzuni na uchungu mwingi” (Marko 14:33). Neno la Kiyunani lililotumika hapa lina maana kwamba kufadhaika kwake kulileta hofu kuu, kama ile watu huwa nayo wakati nywele zao zinaposimama na mwili kutetemeka. Kutolewa kwa sheria kulimfanya Musa kutetemeka kwa woga; kwa hiyo Mwokozi wetu alipatwa na hofu alipoona dhambi ambazo ziliwekwa juu yake.

Mwokozi kwanza alihuzunika, halafu akawa na unyogovu na uzito, na mwisho “huzuni na uchungu mwingi.” Alijawa na fadhaa iliyomtetemesha. Hasa wakati ulipofika wa kuzichukua dhambi zetu, Alitunduwaa kabisa na akapelekwa katika ile hali ya kuchukua mahali pa mwenye dhambi na kusimama mbele za Mungu. Alistaajabu alipomwona Mungu akimwangalia kama mwakilishi wa mwenye dhambi. Alishangaa alipofikiria kuhusu kuachwa na Mungu. Hii iliufadhaisha utakatifu wake, uororo, asili yake ya upendo, na alikuwa “amefadhaika sana” na kuwa na “huzuni mwingi.”

Aidha tunaambiwa ya kwamba alisema, “Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa” (Mathayo 26:38). Neno la Kiyunani “perilupos” linamaanisha kuzungukwa na huzuni. Katika kuteseka kwa kawaida kunaweza kuwa na mwanya wa kuponyoka, nafasi ya kuondokewa na shida. Tunaweza kuwakumbusha walio katika shida kwamba hali yao inaweza kuwa baya zaidi. Lakini katika hali ya Yesu haungeliwaza jambo baya zaidi kuliko hili alilopitia, maana angesema pamoja na Daudi, “Shida za kuzimu zilinipata” (Zaburi 116:3). Mawimbi yote ya Mungu yalijongea juu yake. Juu yake, chini yake, yalimzunguka, kwa nje, na ndani, kote, yote yalikuwa maumivu na hakukuwa na njia ya kuepa huu uchungu na maumivu. Hakuna huzuni ungalipita wa Kristo, na alisema, “Roho yangu ina huzuni nyingi,” alizungukwa na huzuni, “kiasi cha kufa” – hadi alipofikia kifo chake!

Hakufia katika Bustani ya Gethsemane, lakini aliteseka sana kana kwamba alikufa. Aliendele katika maumivu na uchungu yaliyokuwa na makali ya kifo – halafu yakasimama kidogo.

Si shangai kwamba shinikizo la ndani lilifanya jasho ya Bwana wetu iwe kama matone makubwa ya damu. Nimelieleza hili jambo niwezavyo kulingana na uwezo wangu kama mwanadamu.

‘Ni kwa Mungu, na Mungu pekee,
Kwamba huzuni Zake zajulikana vyema.

“Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22:44).

III. Tatu, ni kwa nini Kristo alipitia haya yote?

Nina hakika kwamba watu wengi wanashangaa ni kwa nini Kristo alipitia maumivu haya makuu na kutokwa na jasho ya matone ya damu. Wanaweza kusema, “Ninajua alipitia haya yote, lakini sielewi kwanini alistahili kupitia haya.” Nitakupa sababu tano kwa nini Yesu alipitia hali hii katika Bustani ya Gethsemane.

1.  Kwanza, kutuonyesha utu wake halisi. Usimfikiri kuwa Mungu tu, ingawa hakika yeye ni Mungu, lakini hisi kwamba ni jamaa wa karibu, mfupa wa mfupa wako, nyama ya nyama yako. Jinsi gani anaweza kukuhurumia kwelikweli! Amewekelewa mizigo yako na amehuzunishwa na huzuni zako zote. Hakuna jambo lolote linalotendeka kwako ambalo Yesu halielewi. Hiyo ndiyo sababu inayomwezesha kukuzaidia katika majaribu yako yote. Mshikilie Yesu kama rafiki yako. Atakupa faraja itakayokuwezesha kupitia taabu zote za maisha.

2.  Pili, Mapito aliyopitia katika ile Bustani yanadhihirisha ouvu wa dhambi. Wewe ni mwenye dhambi, Yesu hakuwa mwenye dhambi. Ewe mwenye dhambi, Dhambi zako lazima ziwe za kutisha mno kwa sababu zilisababisha uchungu kwa Kristo. Kuhesabiwa kwa dhambi zetu juu yake kulisababisha jasho ya damu.

3.  Tatu, wakati wake wa majaribu katika ile Bustani uonyesha upendo wake kwetu. Alipitia hofu kwa kuhesabiwa mwenye dhambi mahali petu. Tunawiwa naye kila kitu kwa sababu ya kuteseka kwa ajili yetu, kulipa gharama ya dhambi zetu. Tunastahili tumpende sana kwa kutupenda na upendo mkuu.

4.  Nne, Tazama yesu pale Bustani na ujifunze ukuu wa upatanisho wake. Mimi ni mbaya aji, mimi ni mchafu aji mbele za Mungu. Najihisi tu nastahili kutupwa Jahanamu. Nastaajabu kwamba Mungu hakunitupa pale zamani. Lakini naenda Gethsemane, na ninatazama chini ya ile miti ya mizeituni, na ninamuona Mwokozi wangu. Ndio, ninamuona akigaagaa chini kwa kuhangaika, na ninamsikia akitoa mlio wa maumivu. Naangalia kadokado pale alipokuwa na ninapaona pakiwa pekundu kwa damu yake, halafu uso wake umejaa jasho ya damu. Ninamwambia, “Mwokosi, ni nini mbaya na wewe?” Namsikia akijibu, “Ninateseka kwa sababu ya dhambi zako. ”Na ninatambua ya kwamba Mungu anaweza kunisamehe dhambi zangu kupitia dhabiu aliyonitolea. Kuja kwake Yesu na umwamini. Dhambi zako zitasamehewa kupitia damu yake.

5.  Tano, fikiria kuhusu adhabu ya kutisha itakayokuja kwa wote wanaokataa Damu Yake inayolipia dhambi. Fikiria kwamba Ukimkataa siku moja utasimama mbele za Mungu Mtakatifu na uhukumiwe kwa dhambi zako. Nitakwambia, nikiwa na uchungu katika moyo wangu ninapokwambia, kitakachotokea kwako ikiwa utamkataa Mwokozi, Yesu Kristo. Si katika bustani, lakini katika kitanda, utashangaa na kifo kitakuweza. Utakufa na nafsi yako itachukuliwa ihukumiwe na ipelekwe Jahanamu. Acha Gethsemane ikuonye. Acha mauguzi yake na machozi yake na jasho ya Damu ikusababishe kutubu dhambi zako na umwamini Yesu. Kuja Kwake. Mwamini. Amefufuka kifo na Yuko hai, Ameketi katika mkono wa kuume wa Mungu mbinguni. Kuja Kwake sasa na usamehewe, kabla haujachelewa. Amina.


UNAPOMWANDIKIA DKT. HYMERS NI LAZIMA UMWAMBIE UNAANDIKA KUTOKA NCHI GANI AU HATAJIBU BARUA PEPE YAKO. Ikiwa mahubiri haya yatakubariki tuma barua pepe kwa Dkt. Hymers na umwambie lakini kila mara mjulishe unaandika kutoka nchi gani. Barua pepe ya Dkt. Hymers ni rlhymersjr@sbcglobal.net (bonyeza hapa). Unaweza kumwandikia Dkt. Hymers kwa lugha yeyote, lakini andika kwa kingereza ikiwa unaweza. Ikiwa unataka kumwandikia Dkt. Hymers kupitia posta, anwani yake ni S.L.P. 15308, Los Angeles, CA 90015. Unaweza kumupigia simu kupitia nambari hii (818)352-0452.

(MWISHO WA MAHUBIRI)
Unaweza soma mahubiri ya Dkt. Hymers kila wiki kwa Tovuti
hii www.sermonsfortheworld.com.
Bonyeza hapa kwa “Mahubiri kwa Kiswahili.”

Maandishi ya mahubiri haya hayana hatimiliki. Unaweza kuyatumia bila ruhusa ya
Dr. Hymers. Hata hivyo, mahubiri yote ya video ya Dkt. Hymers, na mahubiri mengine yote
ya video kutoka kwa kanisa yetu, yako na hatimiliki na yanaweza tumiwa tu kwa kuuliza ruhusa.

Wimbo Ulioimbwa Kabla ya Mahubiri na Bw. Benjamin Kincaid Griffith:
“Mateso Yako Yasiyojulikana” (na Joseph Hart, 1712-1768).


MWONGOZO WA

JASHO YA DAMU

THE BLOODY SWEAT

na Dkt. R. L. Hymers, Jr.

“Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22:44).

(Yohana 18:2; Isaya 53:7; Mwanzo 28:17)

I.    Kwanza, ni nini iliyosababisha uchungu na maumivu makuu ya
Kristo kule Gethsemane? Isaya 53:3; Yohana 14:27; 18:1;
Mathayo 26:39, 38, 37; Waebrania 12:2; Isaya 53:6;
I Petro 2:24; Luka 22:44.

II.   Pili, maana ya jasho ya Damu ya Kristo ilikuwa nini?
Luka 22:44; Mathayo 26:37; Isaya 53:4, 11;
Marko 14:33; Mathayo 26:38; Zaburi 116:3; Luka 22:44.

III.  Tatu, ni kwa nini Kristo aliyapitia haya yote? I Petro 2:21;
II Timotheo 3:12; 2:3; Matendo ya Mitume 14:22.